Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imetia saini Mkataba wa Kuijengea Taasisi Uwezo, baina yake na Mhandisi Mshauri-Kampuni ya Gopa Infra ya nchini Ujerumani ikishirikiana na Kampuni ya Superlit Consulting Ltd ya nchini Tanzania, wenye thamani ya Shilingi Bilioni 9.
Mkataba huo umesaini leo Novemba 4, 2024 katika ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu ya SHUWASA katika Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza mara baada ya kusaini Mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, ameeleza kuwa mkataba huo ni wa miaka minne ikiwa ni sehemu mojawapo ya mradi mkubwa wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wenye thamani ya Euro Milioni 76.
“Mhandisi Mshauri huyu atakwenda kutekeleza sehemu mojawapo ya mradi mkubwa wa AFD ambayo ni kuijengea uwezo taasisi, kwanza kufahamu ni maeneo gani yanayohitaji kujengewa uwezo kwa taasisi, watumishi na sehemu zingine katika uboreshaji wa utoaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira,” amesema Mhandisi Katopola.
Ameongeza kuwa Mhandisi Mshauri huyo pia ataisaidia Mamlaka katika kusimamia sehemu zingine za utekelezaji wa mradi wa Majisafina Usafi wa Mazingira Shinyanga.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Kampuni ya Gopa Infra, Stefan Doerner, ameonesha kufurahishwa baada ya kupata fursa ya kufanya kazi nchini Tanzania na kuahidi kusaidia kuijengea uwezo SHUWASA katika kuhakikisha inatoa wa huduma bora za majisafi na usafi wa mazingira.
Itakumbukwa kuwa mnamo Juni 6 2022 Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), zilitia Saini Mkataba wa Ufadhili wa mkopo wa riba nafuu wa Euro Milioni 76 (Takribani Shilingi Bilioni 200), kwaajili ya mradi mkubwa wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga ambao unahusisha kuijengea uwezo taasisi; ujenzi wa mtandao wa majisafi kilomita 287; ukarabati wa mtandao chakavu wa majisafi kilomita 100 na ujenzi wa matangi mawili (Kolandoto-lita 1,500,000 na Didia- lita 250,000).
Aidha, mradi huo unahusisha pia ujenzi wa mitambo minne ya kuchakata tope kinyesi-miwili katika Manispaa ya Shinyanga (Mwagala na Ihapa) na miwili katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga (Kituli na Iselamagazi).
Pia unahusisha ukarabati mkubwa wa mtambo wa kutibu maji Ning’hwa na kufanya tathmini ya ufanisi wa Bwawa la Ning’hwa.